Jogoo
yoh
tazama usiku wa manane, mbalamwezi inang'ara
najistiri nisionekane, nawika kutoa ishara
kuwa tayari kumekucha, sio muda wa kuvuta shuka
amkeni mkajenge Taifa, mpandishe uchumi umeanguka
yapata kumi kasoro, ustaadhi juu ya mimbari
busati na sio godoro, vitabu soma mistari
shustusha waliolala, waabudu swala za mola
wanafurahia amani ilala, Temeke kutwa bastola
kokoriko, nawika nisikike kokote uliko
Afrika bado maskini, madini yanakwenda siko
matabaka juu na chini, makazi mavazi duni
mdhamini aliye 'kitini', miradi anadhidi buni
mwenye ajira anachechema, japo amenyimwa kauli
Mpoto ana mengi ya kusema, lakini amekosa nauli
ni vipi atamuona mjomba, waketi meza moja
amueleze hali halisi, akina sisi wanangoja
wenye hila wanafilisi taasisi, na kuachwa huru
tuendelee kunywa chai na vipande vya sukari guru?
mnatozwa kodi na ushuru, TRA wakeshe baa
kwa starehe na kufuru, ja nani anusuru njaa?
sauti ya jogoo, inawika mitaani
sote tuwe macho tupigane vitani
nasimama kwa mguu mmoja, bila kurusha mbawa
nainama kutunga hoja, kuhusu mgeni na mzawa
wakuja ndo mkurugenzi, mwenyeji nguvu ya ngalawa
ameketi kiti cha enzi, pembeni kombe la kahawa
bado giza totoro, hakuja-pambazuka
Bungeni kuna mgogoro, kwanini mshahara unashuka
wamepaka marashi, ila bado uozo unanuka
wanaunda itifaki, misingi ya haki wanaikiuka
tangu zama za Mkapa, Kikwete alitabiriwa
kabla Nyerere hajafa, Katiba ilikaririwa
kwamba Tanzania imara ni ya Chama, Cha Mapinduzi
Someni vifungu ibara, dadisi fanya uchunguzi
fafanuzi zimefichwa, chambuzi hazieleweki
mgunduzi naumiza kichwa, kwani ujuzi hauzeeki
waganga wanagoma, wagonjwa wanakata roho
madaktari wahitimu, vyuoni wanavua majoho
wanatamani kunichinja, wanifanye kitoweo
ili mradi nisipige mbinja, mawio mpaka machweo
nimishanusurika kwenye tafrija kibao
kwa uwezo wa Mungu nawika wanapatwa na mshangao
sauti ya jogoo, inawika mitaani
sote tuwe macho tupigane vitani
alfajiri imeshajiri, nafanya fujo bandani
nawasitiri hawa utitiri, utafikiri tupo vitani
wananchi wananifuga kizungu, kuku wa kienyeji
nampanda jike yeyote, hata kama akiwa shemeji
hata nikifa mimi, vifaranga watabaki
na sauti kote itafika, hata ukiwa chini ya handaki
jembe imara kwa mkulima, lina chapa sura yangu
tangu zama za bima sipotezi kura yangu
neno Siasa, ni lugha ya mficho yenye maana
ya uongo ulikithiri fitina uovu na laana
furaha kwa mwenye hela, maskini hoi mweisela
viongozi ndio walewale , kingunge na malechela
mwenye akili soma kiundani, nakupa dibaji
usishangae kuona kipato, hakilingani na mahitaji
Vijana, ndo nguvu kazi inayopotea kwa ubishoo
mihadarati na maradhi, faradhi kwa majogoo
sijisifu, ila kiukweli niko tofauti
na wengine waharibifu, Ma'broiler hawatafuti
zaidi ya uchaguzi na uchafuzi wa mazingira
mjasiriamali jitume, usingoje kupewa ajira
sauti ya jogoo, inawika mitaani
sote tuwe macho tupigane vitani
[Mashairibongoflava.blogspot.com]